Mwanafunzi wa Sekondari Afikishwa Mahakamani Akituhumiwa Kuhusika na 'Ugaidi' Uliotokea Katika Mapango ya Amboni Tanga
WAKAZI 10 wa jijini Tanga, akiwemo mwanafunzi wa sekondari wamefikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wakikabiliwa na makosa matano tofauti kuhusu tukio la kuwanyang’anya polisi silaha pamoja na kumuua askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Sajenti Mohamed Rashid Kajembe.
Mwanafunzi aliyefikishwa mahakamani ni Rajab Bakari (19) wa shule ya sekondari na mkazi wa Makorora jijini hapa.
Watuhumiwa
tisa wameelezwa kuwa ni wafanyabiashara, nao ni Mbega Seif (25) maarufu
‘Abuu Rajab’ mkazi wa Kiomoni, Amboni, Ayubu Ramadhani (27) maarufu
‘Chiti’ ambaye ni fundi umeme na mkazi wa Kona Z Kiomoni, Hassani Mbogo
(20) maarufu ‘Mpalestina’ mkazi wa Makorora, Mohamed Ramadhani (19)
mfanyabiashara na mkazi wa Makorora, Sadiki Mdoe (25) maarufu ‘Kizota au
Kisaka’ mkazi Magaoni.
Washtakiwa
wengine ni Saidi Omari (26) mkazi wa Magaoni Tairi Tatu, Nurdin Mbogo
(27) Makorora, Ramadhan Mohamed (18) mkazi wa Donge pamoja na Omari
Harubu Abdala (55) maarufu ‘Ami’ mkazi wa Dunia Hoteli Makorora.
Wakisomewa
mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Aziza Rutala, Wakili wa Serikali,
George Barasa akisaidiana na MariaClara Mtengule, walidai kuwa kosa la
kwanza hadi la tatu linawahusisha washitakiwa namba moja mpaka nane (1
-8) ambao wanatuhumiwa kushiriki kula njama ya kutenda kosa kinyume cha
sheria.
Barasa
alidai kuwa katika maeneo tofauti ya jijini Tanga kati ya Septemba mosi
2014 hadi Januari 26 mwaka huu, washitakiwa wote wanane kwa pamoja
walitenda kosa la kula njama na kufanya kosa la unyang’anyi wa silaha.
Katika
kosa la pili, Barasa alidai mahakamani hapo kwamba mnamo Januari 26
mwaka huu, katika mgahawa wa Jamali ulipo kati ya barabara ya Nne na ya
Tano jijini Tanga, washitakiwa wote wanane waliiba silaha moja aina ya
SMG namba za usajili 14303545 mali ya Polisi na muda mfupi kabla ya
kutenda kosa hilo walitumia visu kumchoma askari H 501 Mwalimu ili
kupata silaha hiyo.
Kosa
la tatu la washitakiwa hao ni unyang’anyi wa kutumia silaha, na
washitakiwa wote wanane wanadaiwa kuwa katika mgahawa wa Jamali uliopo
kati ya barabara ya nne na ya tano waliiba silaha nyingine yenye namba
za usajili 14301230 SMG mali ya polisi na kwamba muda mfupi kabla ya
kutenda kosa hilo walimtishia kwa kutumia nguvu kumnyang’anya silaha PC H
Mansoor kinyume na sheria.
Hata
hivyo, katika kosa la nne ambalo limemhusisha mshitakiwa namba tisa
Nurdin Mbogo wakili huyo wa Serikali, alidai kuwa Februari 6 mwaka huu,
katika sehemu isiyofahamika jijini Tanga, mshtakiwa huyo akijua kuwa
Hassan Mbogo (Mshitakiwa Na. 4) alitenda kosa Septemba mosi 2014 na
Januari 26 mwaka huu alimsaidia kumwezesha kukwepa kushtakiwa na
kuadhibiwa kinyume na sheria.
Katika
hatua nyingine, Wakili wa Serikali Mtengule alisoma shitaka jingine
jipya ambalo liliwahusisha watuhumiwa watatu akiwemo namba 1 na 2 (Mbega
Rajabu na Rajabu Bakari) pamoja na mshtakiwa mwingine Omari Harub
Abdallah ‘Ami’ wakidaiwa kwa pamoja kuhusika kumuua askari wa JWTZ,
Sajenti Mohamed Rashid Kajembe mnamo Februari 13 mwaka huu katika
Mapango ya Amboni Jijini Tanga kinyume cha sheria namba 196 na 197 ya
makosa ya adhabu ya mwaka 2002 .
Washtakiwa hao watatu hawakutakiwa kujibu lolote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo ya mauaji.
Hata
hivyo, washitakiwa wote 10 kwa pamoja wamekana makosa yao, na mahakama
imewanyima dhamana washitakiwa tisa kutokana na makosa waliyotenda
kutokuwa na dhamana.
Mshitakiwa
namba tisa Nurdin Mbogo alishindwa kutimiza masharti ya dhamana baada
ya kutakiwa kutoa Sh milioni moja na mdhamini mmoja mwenye mali
isiyohamishika yenye thamani ya Sh milioni moja.
Washitakiwa wote wamerudishwa rumande hadi kesi hiyo itakapotajwa tena Machi 23 mwaka huu kwa kuwa upelelezi wake haujakamilika.
Mnamo
Februari 13 mwaka huu katika eneo la Amboni Jijini Tanga palizuka
mapigano baina ya askari polisi wakishirikiana na JWTZ dhidi ya watu
wanaodaiwa kuwa ni majambazi, waliokuwa wamejificha kwenye mapango ya
Majimoto.
Katika
tafrani hiyo, kulisababish kifo cha askari wa JWTZ na majeruhi watano
wakiwemo wanajeshi wawili na Polisi watatu, hali iliyozua hamaki kwa
wakazi wa jijini hapa.
Rais
Jakaya Kikwete katika hotuba yake mwezi uliopita alielezea matukio hayo
kuwa ni ya ujambazi, lakini pia yana mwelekeo wa ugaidi na akalitaka
jeshi la polisi kuwasaka watuhumiwa wote na kuwafikisha kwenye vyombo
vya sheria.









0 comments: