Mtuhumiwa Wa Fedha za Escrow Ajichanganya......Ni Yule Kigogo Wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) Ambaye Alihojiwa Jana na Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma
MKURUGENZI Mdhibiti Uchumi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Dk James Diu, amejichanganya mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, kuhusu matumizi halisi ya fedha alizozipokea kutoka kwa James Rugemalira ambazo ni Sh milioni 80.8.
Akijitetea mbele ya baraza hilo, Mkurugenzi huyo ambaye pia aliwahi kushika wadhifa wa Meneja Udhibiti Uchumi katika Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), alikiri kupokea kiasi hicho cha fedha ambacho alidai alikitumia kwa ajili ya matibabu ya mkewe aliyefariki dunia Agosti mwaka jana kwa ugonjwa wa saratani.
Hata
hivyo, katika maelezo yake aliyoyatoa mbele ya Kamati ya Uchunguzi ya
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na tamko lake la mali na
madeni alilolitoa Desemba 30, mwaka jana katika Sekretarieti hiyo,
kiongozi huyo alibainisha kutumia kiasi hicho cha fedha katika kulipia
deni lake la nyumba alilokuwa akidaiwa.
Awali
Wakili wa Sekretarieti hiyo ya maadili, Wemaeli Mtei, akimsomea
mashtaka mkurugenzi huyo, alidai kuwa mlalamikiwa huyo anadaiwa kuomba
na kupokea Sh milioni 80.8 kutoka kampuni ya VIP Engineering and
Marketing Limited kinyume cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Alisema
pamoja na fedha hizo, pia mlalamikiwa huyo anadaiwa kujipatia maslahi
ya kiuchumi kwa kupokea kiasi cha dola za Marekani 25,000 kutoka kampuni
ya Mabibo Beers, Wine and Spirit mali ya Rugemalira, kinyume cha Sheria
hiyo ya maadili, inayokataza kiongozi wa umma kuomba na kupokea maslahi
binafsi.
Aidha
katika hati hiyo ya mashtaka mlalamikiwa huyo pia anadaiwa kupokea dola
za Marekani 10,100 kutoka Kampuni ya Prime Fuel Tanzania Limited ambazo
zote hakuzitamka kama Sheria hiyo ya maadili inavyotaka.
“Mlalamikiwa
ambaye pia kuanzia mwaka 2006 hadi 2011 aliwahi kufanyakazi katika
taasisi ya Serikali ya Ewura inayoshughulika na masuala ya nishati,
alijipatia kiasi hicho cha fedha kutoka kampuni ya VIP yenye hisa
asilimia 30 na kampuni ya IPTL yenye mkataba wa umeme na Tanesco, jambo
linalosababisha mgongano wa kimaslahi,” alisema Mtei.
Shahidi
wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Zahara Guga, alisema
kitendo cha mlalakiwa kuwa na historia ya kufanya kazi EWURA na kupokea
fedha kutoka kampuni ya VIP ambayo inasimamiwa na mamlaka hiyo ni
kinyume na Sheria ya maadili na pia mgongano wa kimaslahi.
Alisema
katika uchunguzi wa kamati hiyo ya uchunguzi, walibaini kuwa
mlalamikiwa alifungua akaunti Februari 4, mwaka jana na kuingiziwa Sh
milioni 80.8 Februari 5, mwaka huo na kampuni ya VIP katika akaunti yake
iliyopo benki ya Mkombozi tawi la Kariakoo.
Akijitetea
mbele ya baraza hilo, Dk Diu, alikanusha kuomba fedha hizo kwa
Rugemalira na kukiri kuwa alipokea kiasi hicho cha fedha ambazo
alipatiwa kama ahadi ya kumsaidia katika matibabu ya mkewe, ikiwa ni
pamoja na kumsafirisha kwenda India kwa matibabu zaidi.
“Rugemalira
ni rafiki yangu wa karibu pamoja na familia yangu, lakini pia nimesoma
naye wakati natafuta shahada yangu ya kwanza Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, mwaka 1982 hadi 1985, alinipatia fedha hizi kama ahadi
sijamuomba, kudai wala kupokea maslahi ya kiuchumi kutoka kwake,” alisisitiza.
Alisema
kutokana na hali mbaya aliyokuwa nayo mkewe, Rugemalira alikwenda
kumjulia hali alipolazwa hospitali ya TMJ na baadaye Sanitarius iliyopo
Mikocheni ndipo alipoahidi kutoa fedha hiyo kama mchango na msaada wa
matibabu na baadaye mazishi baada ya mkewe huyo kufariki dunia.
Aidha
alisema hata katika fomu yake ya tamko la mali na madeni kwa
sekretarieti hiyo, aliyoiwasilisha Februari 30, mwaka jana aliitamka
fedha hizo kuwa ameipokea kutoka kwa Rugemalira.
“Awali sikuona umuhimu wa kuiwasilisha kwa ofisa masuhuli wangu kwa sababu haikuwa zawadi na sikuona umuhimu wa kufanya hivyo,”.
Aidha
alisisitiza kuwa kupokea kwake fedha hizo hakuna mgongano wowote wa
kimaslahi kwa kuwa hana uhusiano wowote wa kibiashara na Rugemalira na
hata kazi yake katika mamlaka ya TCAA haina uhusiano na kampuni za
Rugemalira kibishara.
Hata
hivyo, baadaye akionesha maelezo ya Dk Diu mbele ya kamati ya uchunguzi
alipohojiwa kuhusu kupokea fedha hizo, Wakili wa Sekretarieti hiyo ya
Maadili Getrude Cyriacus, alibainisha kuwa mlalamikiwa huyo alijitetea
kuwa fedha hizo alizitumia kulipia deni la nyumba alilokuwa akidaiwa.
“Hata
katika tamko la mali na madeni aliloliwasilisha mwaka 2012, aliandika
maelezo kuwa anadaiwa Sh milioni 80 za nyumba ambayo haijakamilika
aliyonunua huko Mbezi kutoka kwa Godson Shangwe, na tamko lake la mwaka
jana alibainiha kuwa ametumia fedha hizo alizopewa na Rugemalira
kumalizia deni hilo,” alisema Cyriacus.










0 comments: