Msaada Tutani: Mzazi Anatafuta Mtoto wake Aliyepotea jijini mwanza

Rwanda Wampongeza Rais Magufuli Kwa Kutumbua MAJIPU Bandarini.


WAFANYABIASHARA wa Rwanda wamepongeza hatua zinazochukuliwa na Rais John Magufuli katika Bandari ya Dar es Salaam, kwa kuimarisha ufanisi wa bandari, kukuza biashara baina ya Tanzania na nchi jirani.

Aidha wamesema tangu Rais Magufuli aanze kuchukua hatua hizo, mizigo yao imekuwa salama zaidi na wamefanikiwa kuipata kwa urahisi tofauti na zamani ambapo mingi ilikuwa ikipotea.

Hayo yalielezwa jana na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Akizungumza baada ya kutua nchini akitokea Kigali, Rwanda, Balozi Mahiga alisema pia Rais wa nchi hiyo, Paul Kagame amemhakikishia kuwa ataendelea kushawishi wafanyabiashara wake kutumia Bandari ya Dar es Salaam, ili kukuza uhusiano wa kibiashara uliopo.

“Nilipata bahati ya kuzungumza na wafanyabiashara wa kule... wamepongeza sana hatua zinazochukuliwa na Rais Magufuli pale bandarini kwa sababu wanasema sasa hivi itawasaidia sana kuhakikisha usalama wa mizigo yao,” alisema Blozi Mahiga.

Alisema wafanyabiashara hao pia wameomba mkutano wa pamoja na wenzao wa Tanzania, ili kujadili masuala mbalimbali, ikiwemo fursa za uwekezaji ndani ya Rwanda na Tanzania.

Alisema Rais Kagame anaunga mkono ujenzi wa reli itakayotumika kusafarisha mizigo kwa kuwa ni njia mojawapo ya kukuza uchumi wa nchi hizo mbili rafiki.

Akizungumzia safari yake hiyo, Balozi Mahiga alisema, alienda nchini humo kujadiliana masuala mbalimbali aliyoagizwa na Rais Magufuli kwa Rais wa nchi hiyo, ambapo walijadili masuala matatu, ikiwemo machafuko yanayoendelea Burundi.

Alisema kuhusu machafuko ya Burundi, Rais Kagame alikanusha tuhuma zinazotolewa na nchi hiyo pamoja na jumuiya za kimataifa kuwa anahusika katika kuchochea machafuko hayo.

Kwa mujibu wa Balozi Mahiga, maandamano ya nchi nzima yaliyofanyika wiki iliyopita nchini Burundi ya kuishutumu Rwanda kuhusika na machafuko nchini mwao, yalishitua nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kutokana na baadhi ya maneno ya chuki yaliyokuwa yakitolewa na wananchi hao dhidi ya nchi hiyo.

Alisema hali hiyo, ilihofiwa kwamba ingeweza kuvunja mazungumzo ya kutafuta suluhu yanayoendelea. “Nilimuuliza Rais Kagame kuhusu hili suala, akasema hatachukua hatua yoyote licha ya kwamba wananchi wake wamemlazimisha kufanya kitu."
 Lakini alisema atashiriki katika majadiliano ya kutafuta suluhu ya Burundi. “Sisi tulikuwa tunahofia kuwa huenda akachukua hatua ambazo zingeweza kuleta matatizo na hata mazungumzo yanayoendelea kuvunjika, lakini ameniambia hatachukua hatua yoyote inayoweza kusababisha kuvunjika kwa uhusiano,” alisema Balozi Mahiga.

Hata hivyo, alisema Rais Kagame alilalamikia nchi yake kushutumiwa kwa kutoa mafunzo ya kijeshi kwa wakimbizi wa Burundi, ili kuipindua Serikali ya nchi hiyo na kutaka Jumuiya za Kimataifa, kuwaondoa wakimbizi zaidi ya 70,000 na kuwahamishia nchi nyingine za jirani.

“Aliniambia kuwa kuendelea kuwa na hawa wakimbizi katika nchi yake, kunaweza kumletea matatizo makubwa, kwa sababu amekuwa akilaumiwa sana. Hivyo kuliko lawama, ni bora hizi Jumuiya za Kimataifa zikawaondoa wakimbizi,” alisema.

Alisema kwa mujibu wa Rais Kagame, Rwanda itaendelea kushiriki katika mijadala mbalimbali ya kutafuta suluhu ya Burundi na itahakikisha Burundi inakuwa salama.

Jambo lingine walilozungumza na Rais Kagame ni mkutano wa marais wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, unaotarajiwa kufanyika mwisho wa mwezi nchini Tanzania, ambapo pia alikuwa katika hatua ya mwisho katika kukamilisha ajenda na watakaoshiriki mkutano huo.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu Atangaza Oparesheni Kamata Bodaboda Nchi Nzima


MKUU wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu amewaagiza makamanda wa Polisi kote nchini, kuendesha oparesheni kali ya kuwachukulia hatua za kisheria, waendesha bodaboda wasiotii sheria za usalama barabarani.

Ametaja makosa yatakayosababisha waendesha bodaboda hao kukamatwa kuwa ni pamoja na kubeba abiria zaidi ya mmoja, kupita katika taa nyekundu na kutovaa kofia ngumu.

IGP Mangu alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na maofisa wakuu wa Polisi, wakiwemo makamanda wa Polisi wa mikoa, vikosi na makao makuu katika kikao kazi kilichofanyika Dar es Salaam hivi karibuni ambacho kilifunguliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga.

Alisema waendesha bodaboda wamekuwa wakikaidi kufuata sheria za usalama barabarani, lakini sasa mwisho wao umefika na kuwataka makamanda wa Polisi wa mikoa kote nchini, kutekeleza maelekezo hayo, ili kuleta nidhamu kwa bodaboda katika kufuata sheria za usalama barabarani.

IGP Mangu alisema suala la kufuata sheria za usalama barabarani kwa bodaboda halina mjadala na kila Kamanda ahakikishe kuwa wote wasiofuata sheria na kukaidi, wanakamatwa bila kuoneana muhali kwa kuwa wamekuwa wakisababisha ajali zinazoweza kuzuilika.

“Pamoja na kuendelea kudhibiti uhalifu wa aina zote, natoa maelekezo kwa kila mkoa kuhakikisha unaendesha oparesheni kali dhidi ya bodaboda, ili kupunguza ajali zinazosababishwa na bodaboda.
 “Wengi wao hawataki kufuata sheria na kanuni za usalama barabarani, tusiwaonee muhali maana maisha ya watu ni muhimu sana na jambo la msingi ni kusimamia sheria tu,” alisema IGP Mangu.

Awali akifungua kikaokazi hicho Waziri Kitwanga alilitaka Jeshi la Polisi kuendelea na mapambano yake dhidi ya uhalifu na wahalifu, ili usalama wa raia na mali zao uendelee kuimarika na Watanzania waendelee na shughuli zao za kujiletea maendeleo bila hofu ya kutendewa uhalifu.

Waziri Mkuu Atinga Bandari Ya Tanga....Akutana Na MADUDU Kibao

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa jana jioni (Ijumaa, Februari 19, 2016) alikagua bandari ya Tanga na kumtaka Mkuu wa Bandari ya Tanga (Port Master), Bw. Henry Arika amletee maelezo juu ya ukiukwaji wa manunuzi ya tishari ifikapo leo (Jumamosi) saa 6 mchana.

Waziri Mkuu ambaye aliwasili Tanga jana mchana ili kushiriki mazishi ya baba mzazi wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi. Ummy Mwalimu yaliyofanyika kwenye makaburi ya Mchukuuni, Tanga, aliamua kuzuru bandari hiyo kabla ya kuelekea uwanja wa ndege akiwa njia njiani kurejea Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo fupi, Waziri Mkuu alikataa kuingia ofisini (bandarini) na akataka apelekwe mahali tishari tatu za bandari hiyo zilipo. 
Katika maswali aliyoulizwa na Waziri Mkuu, Bw. Arika alikiri kuwa matishari hayo hayafanyi kazi kama inavyotakiwa kwa sababu yanasubiri kusukumwa na tugboat  (meli ndogo).

"Nataka kesho saa 6 mchana uniletee barua yenye maelezo ni kwa nini mlinunua tishari tatu ndogo badala ya mbiili kubwa wakati mnajua Serikali ilitenga Dola za Marekani milioni 10.113 kwa ajili ya kununua tishari mbili zenye uwezo wa kujiendesha zenyewe  (self propelled) "

“Nataka maelezo ni kwa nini mlizinunua tangu mwaka 2011 lakini zimekaa bila kufanya kazi hadi Novemba mwaka jana? Na kwa nini mnaendelea kutumia hela ya Serikali kwa kukodisha tishari kutoka Mombasa badala ya kutengeneza za kwenu au kufundisha vijana wa Kitanzania? Kwani tunao wahitimu wangapi wa fani hii?" alihoji Waziri Mkuu.

"Taarifa nilizonazo ni kwamba moja ya tishari lilidondoka baharini mkaenda kutafuta huko na kulivuta hadi hapa ndiyo maana yameshindwa kufanya kazi inavyotakiwa," aliongeza.

Katika majibu yake, Bw. Arika alisema wao waliagiza tishari hizo kupitia ofisi ya Bandari makao makuu ambayo iko Dar es Salaam. 
"Pia wakati zinaagizwa sikuwepo hapa Tanga. Nimekuja mwishoni mwa mwaka jana," alisema Mkuu huyo wa Bandari ambaye inaelezwa alitokea Mamlaka ya Bandari Dar es Salaam.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Bibi Mwantumu Mahiza awaite watu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Mamlaka ya Bandari na Jeshi la Polisi wakae na kutafuta mbinu za kudhibiti njia za panya zinazotumika kupitisha sukari ya magendo.

"Mkuu wa Mkoa simamia hawa watu, msaidiane kudhibiti uingizaji wa sukari kwa njia za panya. Kuna majahazi yanaleta sukari kutoka Brazil. Mheshimiwa Rais amepiga marufuku uingizaji wa sukari kutoka nje ili viwanda vyetu vya ndani viweze kuongeza uzalishaji. Dhibitini bandari zote ndogondogo hadi Pangani," alisema Waziri Mkuu.

Alisema changamoto inayoikabili Serikali ni kwamba hata Shirika la Viwango Tanzania (TBS)  au Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) hawawezi kuzikagua sukari hizo na hazijulikani ubora wake licha ya kuwa zinafika kwa walaji.
Waziri Mkuu, Kssim Majaliwa akiongozwa na Mkuu wa Bandari ya Tanga , Henry Arika (kulia kwake) kukagua bandari hiyo Februari 19, 2016.
Matishari matatu ambayo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametaka apewe maelezo kwa maandishi kuwa ni nani aliyeidhinisha mchakato wa manunuzi yake bila kuzingatia viwango na ubora uliokusudiwa na serikali. mheshimiwa Majaliwa alifanya ziara katika bandari ya Tanga Februari 19, 2016. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu)

Mwenyekitiwa Baraza la Michezo Tanzania ( BMT ) Amteua Mohamed Kiganja kuwa Katibu Mtendaji Baada Ya Yule Wa Awali Kufukuzwa


Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania Deonis Malinzi amemteua Mohamed Kiganja kuwa Katibu Mtendaji mpya wa baraza hilo baada ya aliyekuwa anashikilia nafasi hiyo Bw. Henry Lihaya kutenguliwa.

Akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Mwenyekiti Malinzi alieleza kuwa uteuzi huo umekuja baada ya kuona mapungufu ya utendaji kwa aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo.
“Baraza la Michezo Tanzania limefikia maamuzi haya baada ya kutoridhishwa na utendaji wa Bw. Lihaya na hivyo Waziri wa habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye kufanya maamuzi ya kumtengua” alisema Bw. Malinzi

Uteuzi huo umefanyika kwa mujibu wa Sheria ya BMT namba 12 ya mwaka 1967 kifungu namba 5(1) ambacho kinampa mamlaka Mwenyekiti wa BMT kuteua Katibu Mtendaji baada ya kupata idhini ya Waziri mwenye dhamana.

Aidha kabla ya uteuzi huo Kiganja alikuwani Afisa Michezo Mkuu katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuanzia mwaka 2015 mpaka uteuzi wake ulivyofanyika.

Pia aliwahi kufanya kazi kama Afisa Mwandamizi Michezo wa Baraza la Michezo Tanzania na Afisa Michezo Mkuu katika Ofisi wa Waziri Mkuu, anashahada ya kwanza ya Elimu katika masuala ya Michezo na Utamaduni kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Wizara Ya Mambo Ya Nje Yakanusha Kukusanya CV za Wafanyakazi Kwa Lengo la Kuwafukuza


Wizara imepata taarifa zisizo na ukweli zinazoenezwa na kusambazwa na watu wasiokuwa na nia njema kwa Wizara na Serikali kwa ujumla, kuwa Wizara iliyokuwa ya Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliendesha zoezi la kukusanya wasifu(CV) za Wafanyakazi wake kwa lengo la kuwafukuza kazi.
 
 Wizara imesikitishwa na inalaani vikali uvumi wa taarifa hizi na  inakanusha kuwa taarifa hizi hazina ukweli wowote.

Zoezi la kukusanya CV za watumishi ni zoezi la kawaida kwa waajiri na hufanyika Mara kwa mara kwa lengo la kuhuisha sifa na uzoefu wa watumishi wanazopata wakiwa kazini ambapo hatimaye huwekwa kwenye majalada yao binafsi, mwajiri anapaswa kuhakikisha jalada la kila mtumishi lina taarifa zinazoeenda na wakati, hivyo zoezi hili lilifanyika kwa lengo la kuhuisha taarifa za watumishi wa Wizara kama ilivyoelekezwa na mwajiri na si vinginevyo. 
 
Wizara inapenda kutoa ufafanuzi kuwa CV si miongoni mwa nyaraka zinazohitajika katika kumfukuza kazi mtumishi bali mtumishi anafukuzwa kazi kwa kukiuka sheria, kanuni na taratibu za kiutumishi ambapo taratibu maalumu za kinidhamu hufuatwa. 
Katika kipindi husika Wizara haina mtumishi anayetuhumiwa kwa kosa la kinidhamu linaloweza kupelekea kufukuzwa kazi, hivyo taarifa hizi hazina ukweli wowote.

Aidha, Wizara inakemea vikali watu wenye tabia ya kutoa taarifa zisizo na ukweli na zenye kupotosha umma. 
Vilevile Wizara inapenda kuwaasa wananchi kuheshimu sheria na taratibu za Nchi sambamba na kutoeneza taarifa zinazotokana na vyanzo visivyokuwa rasmi au zisizothibishwa na mamlaka husika, kwa kuwa kufanya hivyo ni kukiuka sheria na taratibu za Nchi.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa AfrikaMashariki, Kikanda na Kimataifa.
19 Februari, 2016

Waziri Wa Fedha Na Mipango Akutana Na Wabunge Kutoka Nchini Sweden


Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akizungumzia vipaumbele vya Serikali wakati wa mkutano na Wabunge kutoka nchini Sweden jana jijini Dar es salaam kwa ziara ya kikazi nchini.
***
Waziriwa Fedha na Mipango,Mhe. Dkt. Philip Mpango amekutana na Wabunge wa Sweden katika ukumbi wa Wizara hiyo, kuzungumzia ushirikiano baina Tanzania na Sweden.

Katika mazungumzo yake na wabunge hao ambao wamewasili nchini kwa  ziara ya kikazi, Dkt. Mpango amesema Serikali ya Awamu ya Tano ipo makini na inafanyakazi kwa ufanisi ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma stahiki kutokana na rasilimali zilizopo nchini.

Amesema Serikali imejipanga kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ya ndani ili kuiwezesha nchi kujiendesha yenyewe na kuacha kutegemea misaada ya wahisani.

Aidha, amefafanua kuwa Tanzania imejipanga kuongeza vyanzo vya ukusanyaji mapato pamoja na kuboresha  vyanzo vilivyopo na kuhakikishakila Mwananchi anayestahili kulipa kodi stahiki analipa kwa wakati.

“Ni aibu kwa nchi yenye rasilimali za kutosha Wananchi wake kuishi katika hali ya umasikini, tunachotakiwa ni kuboresha kilimo kwa sababu wananchi wengi ndicho wanachotegemea”, alisema.

Akizungumzia vipaumbele vya Serikali katika mkutano huo, Dkt. Mpango alisema mkazo umewekwa zaidi katika kufanya mapinduzi ya viwanda, ambapo nchi inaanza kuboresha viwanda vilivyopo hususani vile ambavyo hutumia rasilimali zinazopatikana nchini kama zile zinazotokana na kilimo.

Aliongeza kuwa katika kuboresha viwanda pia Serikali ipo katika hatua za kuboresha soko la ndani na nje ya nchi kwa bidhaa zinazozalishwa na viwanda hivyo.

Dkt. Mpango alisema sambamba na kufanya mapinduzi ya viwanda, Tanzania imejipanga kuboresha miundombinu ambapo mpaka sasa kuna miradi mbalimbali ya maendeleo imeanzishwa kama mradi wa umeme vijijini.

Alisema katika suala la umeme, nchi imeazimia kujikita katika uzalishaji wa kutumia vyanzo vingine kama gesi asilia, jua na upepo kuliko kutegemea maji pekee.

Kuhusu sekta ya usafirishaji, Dkt. Mpango amesema Serikali imejipanga kuboresha bandari zote nchini na kuzifanya ziwe za kisasa ili kuhamasisha biashara za ndani na nje ya nchi kupitia bandari hizo.

Hata hivyo, Dkt. Mpango alikiri kuwa uboreshaji wa reli ya kati ni changamoto kwani reli hiyo haiwezi kuboreshwa kwa kutumia fedha za bajeti ya Serikali pekee, hivyo Serikali inajitahidi kutafuta njia za kufanikisha ujenzi huo.

Katika mkutano huo, Dkt. Mpango alizungumzia suala la huduma za kijamii alisema, nchi imejipanga kutoa elimu inayoendana na soko la ajira na Serikali imeanza kutoa elimu ya msingi na sekondari bila malipo ili kuwawezesha wananchi wengi kupata elimu.

Akizungumzia suala la uchumi, Dkt. Mpango alisema hali ya uchumi kwa sasa ni nzuri kwani pato la ndani la Taifa limefika asilimia 7 katika miaka ya hivi karibuni.

Dkt. Mpango alisema ili kufanikisha vipaumbele hivyo, ni lazima maadili na nidhamu ya kazi vifuatwe na watendaji pamoja na watumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu yao.

Aliongeza kuwa Serikali ipo msatari wa mbele kupambana na rushwa na haitosita kuhakikisha watu wote wanaohusika na rushwa wanachukuliwa hatua za kisheria.

Kwa upande  Wabunge kutoka nchini Sweden, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Kenneth Forslund, wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa jitihada mbalimbali zinazochukuliwa katika ukusanyaji wa  mapato ya ndani na kutoa huduma za kijamii.

Tanzania na Sweden zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu ambao umeifaidisha Tanzania katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo kuendeleza miradi ya afya na umeme hususani vijijini, elimu pamoja na kusaidia kukamilisha bajeti ya kila mwaka.

Imetollewa na Msemaji
Wizara ya Fedha na Mipango
Kitengo cha Habari
19.2.2016